Mark 16

Kufufuka Kwa Yesu

(Mathayo 28:1-8; Luka 24:1-12; Yohana 20:1-10)

1 aSabato ilipomalizika, Maria Magdalene, Maria mama yake Yakobo, na Salome walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu. 2 bAsubuhi na mapema, siku ya kwanza ya juma, mara tu baada ya kuchomoza jua, walikwenda kaburini. 3 cNjiani wakawa wanaulizana wao kwa wao, “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe kutoka kwenye ingilio la kaburi?”

4Lakini walipotazama, wakaona lile jiwe, ambalo lilikuwa kubwa sana, limekwisha kuvingirishwa kutoka pale penye ingilio la kaburi. 5 dWalipokuwa wakiingia mle kaburini, wakamwona kijana mmoja aliyevaa joho jeupe akiwa ameketi upande wa kuume, nao wakastaajabu.

6 eYule malaika akawaambia, “Msistaajabu. Mnamtafuta Yesu, Mnazareti, aliyesulubiwa. Amefufuka! Hayuko hapa. Tazameni mahali walipomlaza. 7 fLakini nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro, kwamba, ‘Anawatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtamwona, kama alivyowaambia.’ ”

8 gHivyo wakatoka, wakakimbia kutoka mle kaburini wakiwa na hofu kuu na mshangao. Nao hawakumwambia mtu yeyote neno lolote, kwa sababu waliogopa.

Yesu Anamtokea Maria Magdalene

(Mathayo 28:9-10; Yohana 20:11-18)

9 hYesu alipofufuka alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma alimtokea kwanza Maria Magdalene, yule ambaye alikuwa amemtoa pepo wachafu saba. 10 iMaria akaenda, naye akawaambia wale waliokuwa wamefuatana na Yesu, waliokuwa wanaomboleza na kulia. 11 jLakini waliposikia kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria alikuwa amemwona, hawakusadiki.

Yesu Awatokea Wanafunzi Wawili

(Luka 24:13-35)

12 kBaadaye Yesu akawatokea wawili miongoni mwa wanafunzi wake walipokuwa wakienda shambani akiwa katika sura nyingine. 13Nao wakarudi na kuwaambia wenzao. Lakini hawakuwasadiki wao pia.

Yesu Awaagiza Wale Wanafunzi Kumi Na Mmoja

(Mathayo 28:16-20; Luka 24:36-49; Yohana 20:19-23; Matendo 1:6-8)

14 lBaadaye Yesu akawatokea wale wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa wakila chakula. Akawakemea kwa kutoamini kwao na kwa ugumu wa mioyo yao kwa kutosadiki wale waliomwona baada yake kufufuka.

15 mAkawaambia, “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16 nYeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17 oNazo ishara hizi zitafuatana na wanaoamini: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu; watasema kwa lugha mpya; 18 pwatashika nyoka kwa mikono yao; na hata wakinywa kitu chochote cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”

[Yesu Apaa Kwenda Mbinguni

(Luka 24:50-53; Matendo 1:9-11)

19 qBaada ya Bwana Yesu kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu. 20 rKisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.]

Copyright information for SwhNEN